MRATIBU KITAIFA WA THRDC ATEMBELEA CHAMA CHA WANASHERIA WANAWAKE TANZANIA (TAWLA)

Dar es Salaam, Tanzania

Katika ziara yake ya kuwatembelea wanachama wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) katika Kanda ya Pwani Mkoani Dar es Salaam, Ndugu Onesmo Olengurumwa akiongozana na Mratibu Msaidizi wa THRDC Kanda ya Pwani Bwana Michael Marwa pamoja na Afisa wa Dawati la Wanachama wa THRDC Wakili Joyce Eliezer leo walikitembelea Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (Tanzania Women Lawyers Association – TAWLA).

Katika mazungumzo na Mratibu alipoitembelea TAWLA, Wakili Mary Richard ambaye ni Afisa Programu wa TAWLA alisema, “Tunapenda kushukuru Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) kwa sera ya usalama wa Watetezi waliyotutengenezea. Imetusaidia sana kuboresha mifumo yetu ya usalama. Kwa mfano, tumeweza kuajiri kampuni ya ulinzi [wa ofisi], kuweka Alarm katika vyumba vya kutolea msaada wa kisheria, pamoja na kamera za CCTV.” 

Kwa sasa TAWLA ipo kwenye mchakato wa kutengeneza Mpango Mkakati wake Mpya wa miaka sita (2020 – 2025). Mpango mkakati huu utajikita katika kuangazia misingi ya haki za binadamu na jinsi gani inafanya kazi zake. Hii itasaidia kuondoa changamoto ya kutokueleweka na baadhi ya wadau wa haki za binadamu.

Hivi karibuni, TAWLA inatarajia kusherehekea miaka 30 ya kuanzishwa kwake, na maadhimisho ya miaka 30 ya TAWLA yatakuwa fursa ya kutathmini TAWLA ilipotoka na ilipo sasa.

Akiongelea baadhi ya changamoto wanazokumbana nazo katika kuihudumia jamii, Wakili Marry Richard Afisa Purogramu wa TAWLA alisema,”Unapokuwa unatetea haki za watu, kuna upande mwingine unakanyaga maslahi ya wengine…Baadhi ya watumishi wa umma wanakosa utashi katika kufanya maamuzi ya maswala muhimu yanayohusu haki za binadamu, wengi wao si wawazi. Hii inakwamisha baadhi ya kazi ikiwa pamoja na kukosa vibali au kutokupata vibali kwa wakati”.

Wakili Marry aliongeza kuwa, TAWLA pamoja na changamoto zote wamejitahidi sana kuwa na ofisi katika maeneo ambayo yapo katikati ya makazi ya watu ili kusaidia kutunza usiri wa wateja wanapokwenda kupata msaada katika ofisi za TAWLA.

Wakili Marry pia alikiri kuwa, kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita, mahusiano kati ya asasi za kiraia na serikali yameonekana kulegalega. Hivyo basi, ni vema sasa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) chini ya uongozi wa Mratibu Onesmo Olengurumwa ukatumia mbinu mbalimbali za kuwashauri wanachama wake pamoja na asasi za kiraia kwa ujumla kurejesha mahusiano mazuri na serikali.

“Changamoto ni nyingi tunazokumbana nazo katika utekelezaji wa majukumu yetu ikiwa ni pamoja na kutamkiwa maneno machafu na baadhi ya wateja na hata vitisho vya usalama.”, alichangia pia mmoja wa watendaji wa TAWLA.

Pia Ndugu Onesmo Olengurumwa – Mratibu wa THRDC Kitaifa, aliishauri TAWLA kuwajengea uwezo wanachama wake na kuweka mikakati mahususi ya kuwawezesha wanasheria wanawake. “Wanawake wanakabiliwa na changamoto kubwa za mifumo kandamizi. Baadhi ya sheria ni kandamizi kwa wanawake, hivyo ni vema TAWLA itengeneze kundi kubwa la wanawake watakaokuwa kifua mbele kutetea haki za binadamu Tanzania”, alishauri Ndugu Olengurumwa.

 

Imetolewa na:
Mtandao wa Watetezi Wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC)
Machi 13, 2020