MKUTANO WA MASHIRIKIANO KATI YA THRDC NA WIZARA YA KATIBA NA SHERIA

Dodoma Tanzania

Mtandao wa Watetezi wa haki za Binadamu (THRDC) mnamo tarehe 3 Juni 2021 ulikutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi katika ofisi za Wizara hiyo, Mtumba Jijini Dodoma.

Mkutano huo ulilenga kukuza mashirikiano na uhusiano mwema kati ya Wizara hiyo na Watetezi wote wa Haki za Binadamu nchini, kujadili changamoto za kisheria na za kiutendaji zinazowakabili Watetezi, na kuiomba Wizara kuchukua hatua stahiki dhidi ya changamoto hizo.

Miongoni mwa masuala mengi yaliyoibuliwa na Watetezi wa Haki za Binadamu ni pamoja na kuwepo kwa ushirikiano zaidi kati ya Wizara na Watetezi wa Haki za Binadamu, Serikali kuruhusu raia wa Tanzania na mashirika yasiyo ya kiserikali kufikia Mahakama ya Afrika, Serikali kuridhia mkataba wa Afrika wa haki za Binadamu na watu hasa kwa kundi la watu wenye ulemavu barani Afrika, uboreshaji wa mifumo ya upatikanaji haki, ikiwemo Maboresho ya sheria mbalimbali, Maboresho ya mfumo wa Haki jinai, Ushiriki wa serikali katika mchakato wa kimataifa wa mapitio ya Haki za Binadamu (UPR) na mifumo mwingine ya haki za binadamu huku Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) ukiiomba Serikali irekebishe vifungu vya BRADEA pamoja na kuunda chombo maalumu kwa ajili ya usimamizi wa polisi ili kukuza uwajibikaji.

Katika mkutano huo pia Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) uliweza kuelezea shughuli zinazofanywa na mtandao huo pamoja na wanachama wake zaidi ya 200 walioenea nchini Tanzania bara na visiwani Zanzibar.

THRDC pia ilielezea ushirikiano uliopo kati ya Wizara ya Katiba na Sheria na Watetezi wa Haki za Binadamu nchini katika maswala mbalimbali kipindi cha nyuma ikiwa ni pamoja na kuhimiza mabadiliko ya sheria na Sera muhimu pamoja na kuwajengea uwezo baadhi ya watumishi wa Mahakama katika masuala mbalimbali ya Haki za Watetezi wa Haki za Binadamu nchini huku wakihamasisha kuwepo kwa uwiano baina ya viwango vya kimataifa vya haki za Binadamu na vya viwango vya kitaifa.

Wanachama wa THRDC waliojitokeza katika Mkutano huo ni pamoja na wawakilishi kutoka mashirika ya LHRC, WOWAP, TAWLA, HAKI ELIMU, ZAFAYCO, WOTE SAWA, DOOR OF HOPE, MSICHANA INITIATIVE, na wawakilishi kutoka THRDC.

Kutoka Wizara ya Katiba na Sheria walioshiriki mkutano huu ni Naibu Waziri wa Katiba na sheria Geofrey Pinda, Katibu mkuu Prof. Sifuni Mchome, Naibu Katibu mkuu Dkt Amon Mpanju, Mkurugenzi wa Haki za Binadamu Sarakikya Nkasori, Mkurugenzi wa masuala ya sheria wa Wizara, Pamoja na msajili wa Paralegal na maofisa wengine waandamizi wa Wizara.

Imetolewa na THRDC

Tarehe 3 Juni, 2021