MAHAKAMA YA AFRIKA MASHARIKI (EACJ) YASIKILIZA MAOMBI YA MCT, THRDC NA LHRC YA KUFUTA KUSUDIO LA SERIKALI YA TANZANIA KUKATA RUFAA YA KESI YA SHERIA YA HUDUMA ZA HABARI (2016)

MAHAKAMA YA AFRIKA MASHARIKI (EACJ) YASIKILIZA MAOMBI YA MCT, THRDC NA LHRC YA KUFUTA KUSUDIO LA SERIKALI YA TANZANIA KUKATA RUFAA YA KESI YA SHERIA YA HUDUMA ZA HABARI (2016)

Leo tarehe 21 Mei 2020 majira ya saa 3:30 asubuhi, Mahakama ya Afrika Mashariki (EACJ) kitengo cha rufaa kilichopo jijini Arusha, Tanzania ilisikiliza maombi ya Baraza la Habari Tanzania (MCT), Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) ya kuiomba mahakama kufuta kusudio la Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kukata rufaa dhidi ya uamuzi wa mahakama hiyo wa kesi kupinga baadhi ya vifungu vya Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 (Media Services Act, 2016), uliowapa ushindi MCT, THRDC na MCT mnamo tarehe 28 Machi 2019.

Kesi hii imesikilizwa leo kwa njia ya mtandao wa video (Videoconference) mbele ya jopo la majaji watano wa rufaa wa Mahakama ya Afrika Mashariki na kuongozwa na Raisi wa Mahakama hiyo Emmanuel Ugirashebuja akisaidiana na Liboire Nkurunzinza, Aaron Ringera, Geoffrey Kiryabwire na Sauda Mjasiri.

Upande wa MCT, THRDC na LHRC uliwakilishwa na Mawakili Fulgence Massawe na Jebra Kambole. Wakati upande wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Tanzania uliwakilishwa na Mawakili Alicia Mbuya, Abubakari Mrisha na Stanley Kalokola.Itakumbukwa kuwa, mnamo mwezi Januari mwaka 2017, kesi hii ilifunguliwa kwa pamoja na Baraza la Habari Tanzania (MCT), Kituo cha Sheri na Haki za Binadamu (LHRC) na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) katika Mahakama ya Afrika Mashariki (EACJ).

Na baadaye mnamo tarehe 28 Machi 2019 Mahakama hiyo ilitoa hukumu iliyowapa ushindi MCT, THRDC na LHRC na kusema kuwa baadhi ya vifungu vya Sheria ya Huduma ya Habari ya mwaka 2016 vinakiuka Mkataba unaoanzisha Jumuiya ya Afrika Mashariki na kuamuru vifutwe.

Lakini kwa kutoridhika na uamuzi huo wa Mahakama ya Afrika Mashariki, upande Serikali ya Tanzania ulitoa taarifa ya nia ya kukata rufaa mnamo tarehe 11 Aprili 2019. Hata hivyo upande wa Serikali ya Tanzania haukuwahi kukata rufaa ndani ya siku 30 tangu tarehe ya kuonesha nia la kukata rufaa.Hivyo basi kufuatia kuchelewa kwa kukata rufaa, mnamo mwezi Desemba 2019, mawakili wanaoyawakilisha mashirika ya MCT, THRDC na LHRC waliwasilisha maombi ya kufuta kusudio la Serikali ya Tanzania ya kukata rufaa.

Baada ya jopo la majaji wa Mahakama ya Afrika Mashariki kusikiliza maombi hayo leo, Mahakama imeahidi kutoa uamuzi wake rasmi ifikapo tarehe 9 Juni 2020.

Akiongea na waandishi wa habari baada ya kusikilizwa kwa kesi hii asubuhi ya leo, Wakili Fulgence Massawe ameeleza kuwa,

“Leo Mahakama ya Afrika Mashariki kitengo cha rufaa imesikiliza maombi yetu ya kufuta taarifa ya kutaka kukata rufaa ya upande wa Serikali ya Tanzania…Kwa mujibu wa kanuni za mahakama hii, rufaa hupaswa kukatwa ndani ya siku 30 tangu kuwekwa kwa notisi ya kutaka kukata rufaa. Kwahio leo baada ya kusikiliza maombi yetu, mahakama imeahidi itatoa hukumu yake mwezi wa Sita tarehe 9 mwaka huu.”

Pia Wakili Fulgence Massawe akielezea umuhimu wa kufungiliwa kwa kesi hii hapo awali aliongeza,

“Tulifungua kesi hii mnamo mwaka 2017 kupinga baadhi ya vifungu vya Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016, kwakuwa inaminya uhuru wa habari na uwanja mpana wa waandishi na vyombo vya habari kujiachia kwaajili ya wananchi kupata habari.”

Imetolewa na:
Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC),
Mei 21, 2020
Dar es Salaam1 Comment

Comments are closed.