MAADHIMISHO YA 7 YA SIKU YA WATETEZI WA HAKI ZA BINADAMU TANZANIA 2021

MAADHIMISHO YA 7 YA SIKU YA WATETEZI WA HAKI ZA BINADAMU TANZANIA 2021

Dar es Salaam, Tanzania

Leo tarehe 2 Julai 2021, Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) tumesheherekea kwa mara ya 7 Siku ya Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (Defenders’ Day). Maadhimisho haya yamefanyika katika ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam.

Mgeni rasmi aliyealikwa katika hafla yetu alikuwa Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa lakini aliwakilishwa na Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi.

Akisoma hotuba kwa niaba ya Mgeni rasmi Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa, Waziri Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi alifungua rasmi maadhimisho yetu ya 7 ya Siku ya Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania kwa kusema, “Namshukuru sana Mhe.Waziri Mkuu kwa kunipa heshima hii kubwa ya kumwakilisha. Maadhimisho haya ni muhimu sana kwangu kutokana na ukweli kwamba sehemu kubwa ya majukumu yanayotekelezwa na asasi za Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), zinaratibiwa na Wizara ya Katiba na Sheria.”

Mhe. Waziri wa Katiba na Sheria Prof. Palamagamba Kabudi akihutubia wageni waalikwa katika hafla ya Maadhimisho ya 7 ya Siku ya Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania iliyoandaliwa na THRDC

Aidha, Waziri Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi aliendelea kwa kusema, “Tasnifu yangu ya udaktari wa sheria inahusu Haki na Uhuru wa raia nchini Tanzania, Kenya na Uganda. Kwahio ni eneo ambalo nalielewa na nalifahamu vizuri sana…Mimi si mgeni katika Asasi za Kiraia. Na mara nyingine vinapokuja vizazi vipya yafaa tuvikumbushe kwamba, sisi ndio tulikuwa waanzilishi wa mashirika kama vile Legal and Human Rights Centre na Lawyers’ Environmental Action Team (LEAT).”

Naye Wakili Onesmo Olengurumwa, Mratibu Kitaifa wa THRDC alitambua mchango wa serikali kwenye sekta ya AZAKi na alikuwa na haya ya kusema, “Tunaipongeza serikali kwa kuendelea kukaa karibu na AZAKi, ingawa bado tunasisitiza ukaribu huu uendelee kuwepo na kuwekwe mikakati ya kudumu isiwe ya kubahatisha bahatisha. Na kuwepo na utaratibu utakaohakikisha AZAKi haziachwi nyuma.”.

Baadae, wageni wengine wa meza kuu nao walitoa salamu zao kwa wageni waalikwa. Dkt. Camillius Kassala, ambaye alikuwa mwakilishi wa Katibu Mkuu Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (TEC) aliwasalimu wageni waalikwa na kutoa ujumbe mfupi, “Msingi wa Baraza la Maaskofu Katoliki (T.E.C) katika kujihusisha na masuala ya haki za binadamu ni msingi uliosimama juu ya imani katoliki ambayo ipo katika neno la Mungu.”

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya NGOs Bw. Richard Sambaiga alisema, “Niishukuru THRDC kwa kuandaa tukio hili ambalo sio tu kwamba ni kumbukumbu ya tangu kuanzishwa kwake lakini pia inatoa fursa ya kutafakari mwenendo wa utendaji wa shirika na wadau kwenye sekta kwa ujumla…Tunaendelea kujenga mazingira wezeshi kwa Asasi za Kiraia. Na pia mgeni rasmi, hizi Asasi za Kiraia zimetoa ombi kwako kwamba, wanaomba mchango wao nao utambuliwe kwenye kazi na taarifa mbalimbali za serikali. Hilo ni jambo ambalo hata sisi kwenye uratibu wa mashirika tunalisisitiza sana.”.

Balozi wa Sweden nchini Tanzania Mhe. Anders Sjorberg naye aliipongeza THRDC kwa uandaaji wa halfa hii ya maadhimisho ya 7 ya siku ya watetezi wa haki za binadamu na kuongezea kuwa, “Utetezi wa haki za binadamu nchini Tanzania ni eneo ambalo Ubalozi wetu unaliunga mkono. Kwa ujumla, napenda kuzipongeza Asasi za zote za Kiraia nchi kwa kazi zenu.”

Mhe. Balozi Anders Sjorberg wa Ubalozi wa Sweden nchini Tanzania, akizungumza.

Pia Mbunge wa Viti Maalum Neema Lugangira alisimama na kutoa hotuba yake fupi, “Nafarijika kuwa sekta ya AZAKi imenikubali na imenipokea kama mwakilishi wenu bungeni. Nadhani hii pia inatokana na jitihada zangu binafsi za kuendela kuwashirikisha, kujifunza na kuwa pamoja nanyi. Huu ni mwanzo mzuri kwa maslahi mapana ya Taifa letu.”

Baadae, Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi na wageni wa meza kuu kwa pamoja walizindua rasmi Kijitabu cha Mpango Mkakati wa Asasi za Kiraia nchini Tanzania wa kushiriki katika Kutekeleza Mpango wa Tatu wa Maendeleo ya Taifa wa Miaka mitano (2021/22 – 2025/26). Mpango huu wa serikali unalenga kukuza uchumi wa taifa pamoja na kuboresha maisha ya watanzania ndani ya miaka mitano ijayo, na hivyo Asasi za Kiraia nazo zimezindua kijitabu cha Mpango Mkakati utakaoziongoza kuunga mkono juhudi za Mpango mama wa Serikali.

Mhe. Waziri Prof. Kabudi katika picha ya pamoja na Wageni Maalum wa Meza kuu wakishikilia vijitabu vya Mpango Mkakati wa AZAKi wa Kuunga Mkono juhudi za Utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano ijayo (2021/22 – 2025/26)

Baada ya uzinduzi huo, THRDC iliyatunuku mashirika 11 tuzo za umahiri wao katika kuchangia maendeleo ya taifa kwenye sekta mbalimbali, lakini pia tuzo hizo zikiwa kama chachu ya kuyafanya mashirika hayo yaendeleze juhudi zao katika kuunga mkono utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka mitano (2021/22 – 2025/26).

Mashirika hayo ni;
1) Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC); kilitunukiwa tuzo ya umahiri wake kwenye utoaji wa huduma za misaada ya kisheria kwa wananchi ndani ya Tanzania bara na visiwani Zanzibar.

2) Sanitation and Water Action (SAWA); ilitunukiwa tuzo ya umahiri katika utuoaji wa huduma za maji safi na salama.

3) Lawyers’ Environmental Action Team (LEAT); ilitunukiwa tuzo ya umahiri kwenye utetezi wa haki za kimazingira.

4) Rafiki SDO; ilitunukiwa tuzo ya umahiri katika utoaji wa ajira pamoja na fursa za kujiajiri kwa vijana na wanawake.

5) Agape AIDS Control Program; ilitunukiwa tuzo ya umahiri kwenye ulinzi wa watoto wa kike dhidi ya ukatili wa kijinsia na maambukizi ya UKIMWI.

6) Tanzania Horticultural Association (TAHA); ilitunukiwa tuzo ya umahiri katika sekta ya kilimo-biashara cha mazao ya matunda, maua na mbogamboga.

7) Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (T.E.C); lilitunikiwa tuzo ya umahiri wao katika kutoa huduma za afya nchi nzima.

8) Tanzania Women Lawyers’ Association (TAWLA); ilitunukiwa tuzo ya umahiri wake kwenye utetezi wa haki za wanawake na watoto kwa kuwapa huduma bure za misaada ya kisheria.

9) SOS Children Villages – Tanzania; ilitunukiwa tuzo ya umahiri wake kwenye utetezi wa haki za watoto, hususan malezi ya watoto yatima na wale wanaoishi kwenye familia maskini.

10) Tanzania Natural Resources Forum (TNRF); ilitunukiwa tuzo ya umahiri wake katika utetezi wa haki za mali asili, madini na ardhi kote nchini.

11) HakiElimu; ilitunukiwa tuzo ya umahiri wake kwenye sekta ya elimu na utetezi wa haki ya watanzania kupata elimu bora.

Mwishoni, Mhe. Waziri Prof. Kabudi aliongozana na wageni wa meza kuu kupita kwenye mabanda ya maonesho ya asasi za kiraia nje ya ukumbi.

Wakati wa mchana mara baada ya wageni waalikwa kupata chakula cha mchana, THRDC iliendesha mada kwa lisaa limoja kuhusu mchango wa Asasi za Kiraia (AZAKi) kwenye maendeleo ya Taifa. Mjadala huu ulilenga kuibua mijadala kuhusu uhitaji wa michango ya AZAKi kutambuliwa na serikali.

#SikuYaMaadhimishoYa7YaWateteziTz2021

#7thHRDsDayTz2021

Imetolewa na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC),
Leo tarehe 2 Julai, 2021