KESI YA TITO MAGOTI NA THEODORY GIYAN IMETAJWA KWA MARA YA 4 LEO MAHAKAMANI KISUTU

Dar es Salaam – Tanzania

Kesi ya utakatishaji fedha namba 137 ya mwaka 2019 inayowakabili Afisa Programu wa Elimu kwa Umma wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Tito Magoti pamoja na mwenzake Theodory Giyan mtaalamu wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), imetajwa kwa mara ya 4 leo Februari 5, 2020 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam mbele ya Mheshimiwa Hakimu Mkazi Janet Mtega.

Washtakiwa wote wawili, Tito Magoti na Theodory Giyan walifikishwa mahakamani ili kuhudhuria kutajwa kwa kesi yao. Upande wa Serikali uliongozwa na Wakili mwandamizi wa serikali Renatus Mkude akisaidiwa na wakili Monica Mbogo wa serikali. Wakati upande wa utetezi (Tito Magoti na Theodory Giyan) uliwakilishwa na Jopo la mawakili 10 wakiongozwa na wakili Alex Mgongolwa. Pia Associate Protection Officer: Emergency Support and Rescue mwanasheria Paul Kisabo wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) alifika mahakamani hapo kufuatilia kesi hiyo kwa ukaribu.

Upande wa Jamhuri ulianza kwa kusema kwamba kesi hiyo imekuja kutajwa na kwamba upelelezi umefikia hatua nzuri. Wakili Renatus aliendelea kuieleza mahakama kwamba kwa ajili ya kumbukumbu za mahakama, upande wa Jamhuri unapaswa kueleza hatua ambazo upelelezi umefikia, lakini ukweli ni kwamba upelelezi haujakamilika licha ya kufikia hatua nzuri. Ameeleza kuwa hii ni kutokana na sababu zinazopelekea upelelezi kuhusisha hatua za ndani na nje ya nchi kulingana na msingi wa makosa yenyewe hivyo upelelezi kwa ngazi ya hatua za nje ya nchi ni lazima uzingatie hatua za kisheria ambazo kwasasa zinaendelea.

Wakili wa upande wa utetezi Alex Mgongolwa akijibu hoja za jamhuri ameiambia mahakama kwamba kiini cha shauri kinahusisha teknolojia hivyo hatutegemei maajabu ili upelelezi kukamilika kwa sababu tuhuma za washtakiwa zinahusiana na umiliki wa kompyuta.

Wakili Alex alisema kwamba upande wa Jamhuri unapaswa kueleza hatua walizofikia katika upelelezi na kama ni wa kisayansi wanapaswa kusema ni sayansi gani ili mahakama ifahamishwe.

Ikiwa watuhumiwa walikutwa na kompyuta pamoja na programu wanayodaiwa kuimiliki, maana yake ni kwamba upande wa upelelezi wanajua kila kitu kuhusu watuhumiwa hivyo tangu Desemba 24, 2019 ni dhahiri upelelezi unapaswa kuwa umekamilika.

Wakili Massawe ameiambia mahakama kwamba msingi wa kesi umejikita kwenye umiliki wa kompyuta. Maana ya kumiliki ni kuwa na kitu chini ya umiliki wako. Hivyo amehoji kwanini upelelezi usikamilike mapema ikiwa watuhumiwa wanadaiwa walikutwa na kile wanachodaiwa kukimiliki. Pia Wakili Massawe ameigusia Sheria ya Taifa ya Huduma za Upelelezi inayosema kwamba “investigate before you prosecute”.

Naye Wakili Mtobesya amesema kwamba dhana ya makosa ni kwamba walikutwa wanamiliki kompyuta na ukisoma maelezo ya makosa yote matatu yanasema watuhumiwa walikutwa na vitu vyote vinavyoadaiwa kuwa walikuwa wanavimiliki. Hivyo tunahitaji mahakama iambiwe ni wapi upelelezi huo unatafutwa na lini utakamilika na ni nini hasa wanachunguza kama vitu vyote waliwakuta wanavyo.

Wakili Mtobesya ameiambia mahakama pia kwamba kwa mujibu wa kifungu namba 178 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, jamhuri wakikamilisha upelelezi wanapaswa kuijulisha mahakama ili iweze kutoa amri ya kesi kuanza kusikilizwa mbele ya Mahakama ya Rushwa na Uhujumu Uchumi. “Sasa ni lini watakamilisha upelelezi ili kesi ianze kusikilizwa?”, Amehoji Wakili Mtobesya.

Pia Wakili Joanita Mutayoba ameiambia mahakama kwamba mara ya mwisho jamhuri walidai upelelezi uko katika hatua za mwisho. Leo kwa jinsi walivyoeleza ni kama vile upepelezi bado haujakamilika. “Watuambie ieleweke upelelezi uko katika hatua gani?”, alihoji Wakili Joanita.

Wakili mwandamizi wa serikali Renatus Mkude alijibu hoja zilizotolewa na mawakili wa utetezi kwa ujumla kwamba ni kweli upelelezi ulikuwa umefikia hatua nzuri. Licha ya kueleza hivyo lakini ukweli ni kwamba upelelezi haujakamilika na bila kujali tumefikia wapi lakini kwa ‘vyovyote vile upelelezi bado haujakamilika’. “Pia sio tu umiliki wa kompyuta isipokuwa ni umiliki wa kompyuta na program yake. Haya mambo yanahitaji utaalamu. Kile walichokutwa nacho ni programu ya kompyuta”, alisema Wakili Mkude.

Aidha wakili Mkude alidai kwamba hakuna kifungu katika sheria yetu kinachoeleza mtuhumiwa asikamatwe mpaka upelelezi ukamilike. Wakili Mkude alidai kwamba kuna masuala ya kiteknolojia katika msingi wa hati ya mashtaka iliyoko mahakamani ambayo yanahitaji utaalamu zaidi. Hayo mambo ya kiteknolojia yanahusisha upelelezi wa ndani na nje ya nchi hivyo yanahitaji kufuata msingi wa kisheria ili kupata ushahidi utakaokamilisha upelelezi.

“Tunafahamu washtakiwa wako ndani. Tumefanya yale yanayohitaji kufanyika kwa haraka. Hii yote ili kutenda haki. Lakini katika kufanya hivyo upelelezi ndio hivyo bado haujakamilika”, aliongeza Wakili Mkude.

Baada ya Mahakama kuzingatia hoja za pande zote mbili, imeahirisha kesi hiyo mpaka tarehe 19 Februari 2020 ambapo kesi hiyo itatajwa tena na upande wa Jamhuri unapaswa kuieleza mahakama hatua kamili za upelelezi ulipofikia. Kesi hiyo imehudhuriwa na mamia ya watu mahakamani hapo wakiwemo mabalozi, watetezi mbalimbali wa haki za binadamu na wananchi kwa ujumla.

Ikumbukwe kwamba, Tito na Theodory wanatuhumiwa kwa makosa matatu ambayo ni: kushiriki genge la kihalifu, kumiliki programu ya kompyuta kwa lengo la kufanya uhalifu na kutakatisha fedha kiasi cha shilingi milioni 17 za kitanzania.

Tito Magoti alikamatwa na watu wasiojulikana mnamo Desemba 20, 2019 akiwa eneo la Mwenge jijini Dar es Salaam na kutokomea naye mahali pasipofahamika, hali ambayo ilizua taharuki na kuibua hali ya sintofahamu miongoni mwa mashirika ya haki za binadamu nchini na ya kimataifa ambayo yalishinikiza watekaji hao kumuachia Tito Magoti pamoja na mwenzake mara moja.

Hata hivyo, tukio la kutekwa kwa Tito na mwenzake lilionekana kuwa na mvutano baada ya kamanda wa kanda maalum ya Dar es Salaam na kamanda wa mkoa wa kipolisi kinondoni kutoa taarifa zinazokinzana kuhusu kushikiliwa kwa Tito Magoti na Theodory Giyan.

Tito Magoti na mwenzake Theodory Giyan, kabla ya kufikishwa mahakamani walishikiliwa kwa zaidi ya masaa 72 huku taarifa za kukamatwa kwao zikiwa hazijawekwa wazi kinyume na sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.

Mnamo Disemba 24, 2019 Tito Magoti na mwenzake walifikishwa mbele ya mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kusomewa mashtaka matatu ambayo hayana dhamana kwa mujibu wa sheria za Tanzania.

Kesi hiyo ilitajwa kwa mara ya pili Januari 7, 2020 ambapo upande wa upelelezi ulidai kwamba upelelezi umefikia hatua inayoridhisha. Mahakama iliahirisha kesi hiyo na Januari 21, 2020 ilitajwa kwa mara ya 3 ambapo bado upande wa upelelezi ulidai kwamba, upelelezi unaridhisha japo bado haujakamilika.

#JusticeForTitoMagoti
#JusticeForTheodory

Imetolewa na:
Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania – THRDC
Tarehe: 05/02/2020