KESI DHIDI YA SPIKA JOB NDUGAI NA CECIL MWAMBE KUTAJWA KESHO

KESI DHIDI YA SPIKA JOB NDUGAI NA CECIL MWAMBE KUTAJWA KESHO

Dar es Salaam, Tanzania

Kesi iliyofunguliwa na shirika la Civic and Legal Aid Organization (CILAO) kuomba tafsiri ya Mahakama Kuu kufuatia kitendo cha Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kumrejesha Bungeni Ndg. Cecil Mwambe itatajwa kesho tarehe 03 Juni 2020 sa 03:00 asubuhi mbele ya Jaji Maige, Jaji Magoiga na Jaji Kulita, Mahakama Kuu ya Tanzania Dar es Salaam.

Kesi hiyo namba 12 ya mwaka 2020 mwanzo ilifunguliwa katika Mahakama Kuu ya Tanzania Masijala ya Arusha mnamo tarehe 19 Mei 2020. Mnamo Mei 28, 2020 kesi hiyo ilihamishiwa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masijala ya Dar es Salaam. Katika kesi hiyo washitakiwa ni Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Yustino Ndugai, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Ndanda Ndg. Cecil Mwambe kufuatia kitendo cha Spika kumruhusu Cecil Mwambe kuendelea kuhudhuria vikao vya bunge.

Shirika la CILAO lilifungua kesi hiyo kuiomba Mahakama Kuu kutoa tafsiri kuhusu kitendo cha Spika kumrejesha bungeni aliyekuwa Mbunge wa jimbo la Ndanda Ndg. Cecil Mwambe wakati alishajihuzuru nafasi yake ya ubunge na uanachama wa Chadema na kuhamia Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Shirika la CILAO kabla ya kufungua kesi hiyo, lilikusanya maoni ya watanzania waliofikia 3,000 wote walipinga kitendo cha Spika kumrejesha bungeni Ndg. Cecil Mwambe. CILAO ilifungua kesi hiyo kwaniaba ya watanzania na watu wote wanaopenda utawala wa Sheria katika nchi yetu.

SABABU ZA KUFUNGUA KESI HIYO NI ZIFUATAZO

1) Kwamba Ibara ya 26(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1977, inatoa wajibu wa kila raia kuitii Katiba pamoja na Sheria za Jamhuri ya Muungano. Spika wa Bunge, Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na aliyekuwa Mbunge wa jimbo la Ndanda Bw Cecil Mwambe wanawajibu pia wa kuitii Katiba ikiwemo Ibara ya 71(1)(f) ya Katiba pamoja na kifungu namba 6C(2) na 6C(3) cha Sheria ya Vyama vya Siasa [Sura ya 288 Toleo la Mwaka 2002].

2) Kwamba kwa mujibu wa Ibara ya 71(1)(f) ya Katiba na kifungu namba 6C(2) na 6C(3) cha Sheria ya Vyama vya Siasa [Sura ya 288 Toleo la Mwaka 2002], Mbunge atakoma kuwa mbunge endapo atajihuzuru nafasi yake ya ubunge na kuhamia chama kingine kama ambavyo Bw Cecil Mwambe alijihuzuru.

3) Kwamba kwa uzoefu wa uendeshaji wa kibunge na kama ambavyo ilishawahi kutolewa ufafanuzi na Spika kwenye kesi ya Abdalah Mtulia, Mwita Mwikabe, Dr. Godwin Mollel, Katani Ahmad Katani na wengine wengi, yanadhihirisha wazi kwamba Mbunge akitangaza kujihuzuru ubunge na kuhamia chama kingine, Mbunge huyo anakoma kuwa mbunge.

4) Kwamba Spika alishathibitisha kujihuzuru kwa Mbunge Mwambe na alitoa maagizo ya kusitishwa mshara wa Mwambe baada ya Februari 15, 2020.

CILAO inaamini Mahakama Kuu itatenda haki katika kutoa tafsiri sahihi ya Katiba na Sheria ya Vyama vya Siasa.

Shirika la CILAO linawashukuru watanzania wote waliotoa maoni yao kuhusu kupinga kitendo cha Spika kumrejesha bungeni Ndg. Cecil Mwambe. Tunawashukuru watanzania wote waliotoa maoni na tunaamini Mahakama Kuu itawatendea haki wananchi katika kesi hii muhimu katika kuhakikisha utawala wa Sheria unazingatiwa.

Imetolewa na:
CIVIC AND LEGAL AID ORGANIZATION (CILAO)
Juni 02, 2020