JAMHURI YAONDOA SHAURI MAHAKAMANI DHIDI YA MWANDISHI SEBASTIAN ATILIO

Iringa – Tanzania

Leo Machi 5, 2020 Jamhuri imeondoa shauri katika Mahakama ya Wilaya ya Mufundi dhidi ya mwandishi wa habari Sebastian Atilio (pichani). Kesi yake ilikuwa imepangwa kutajwa tena leo Machi 5, 2020. Hata hivyo, Wakili wa Jamhuri ameieleza mahakama kwamba hawana nia ya kuendelea na kesi hiyo tena kwa mujibu wa kifungu namba 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai Sura ya 20 [Toleo la mwaka 2002].

Kukamatwa kwake
Mwandishi Sebastian Atilio alikamatwa mnamo Septemba 6, 2019 Mafinga mjini stendi wakati anakata tiketi kusafiri kwenda Bungeni Dodoma kufanya shughuli zake za uandishi.

Baada ya kukamatwa alipelekwa kituo kikuu cha polisi Wilaya ya Mufindi kilichopo Mafinga na kuhojiwa kuhusu kutoa taarifa za uongo kwenye akaunti yake ya ukurasa wa Facebook na kwenye kundi la WhatsApp kwamba “wawekezaji wameenda kupima ardhi kwenye kijiji cha Ifupila” na pia alihojiwa kwanini anafanya kazi za uandishi bila ya kuwa na kibali cha Bodi ya Waandishi wa Habari Tanzania.

Mashtaka Dhidi yake
Mwandishi aliendelea kushikiliwa kituo cha polisi hadi Septemba 9, 2019 ambapo alifikishwa mbele ya Mahakama ya Wilaya ya Mufindi na kusomewa mashtaka mawili. Moja: kutoa taarifa za uongo kinyume na kifungu namba 16 cha Sheria ya Makosa ya Mtandaoni, 2015. Pili: kufanya kazi za uandishi wa habari bila ya kuwa na kibali kutoka Bodi ya Waandishi wa Habari Tanzania kinyume na kifungu namba 50(2)(b) cha Sheria ya Vyombo vya Habari, 2016.

Mahakama ilimnyima dhamana mwandishi huyo hadi Septemba 27, 2019 ambapo alipatiwa dhamana chini ya usimamizi wa wakili Chengula Emmanuel wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC).

Mwenendo wa Kesi hiyo
Kesi ya mwandishi huyo imetajwa mara 9 mbele ya Mahakama ya Wilaya ya Mufindi bila kusikilizwa hata mara moja. Leo Wakili wa Jamhuri ameieleza mahakama kwamba kwa mujibu wa kifungu namba 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, Jamhuri haina nia tena ya kuendelea na kesi hiyo.

Mwisho
Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) umefatilia kwa ukaribu mwenendo wa kesi hii na kugundua kwamba, kesi hii imetajwa kwa kusuasua bila kusikilizwa ambayo ni dalili ya kwamba mwandishi Sebastian Atilio alikamatwa bila upelelezi kukamilika na hivyo kupelekea kesi yake kutosikilizwa hata mara moja.

THRDC inatambua kwamba, Bodi ya Waandishi wa Habari Tanzania haijawahi kuundwa kisheria. Hata hivyo, ikumbukwe kuwa, kwa sasa, chombo kinachoratibu maadili ya waandishi wa habari Tanzania ni Baraza la Habari Tanzania (MCT).

Simu za mwandishi huyo bado zinashikiliwa polisi, hivyo THRDC inatoa wito kwa jeshi la polisi kumrudishia simu zake mwandishi huyo ili aendelee na shughuli zake kwa kutumia vifaa vyake.

Mnamo Februari 25, 2020 Mtandao ulitoa ripoti ya uangalizi wa kesi ya mwandishi Erick Kabendera na moja ya mapendekezo yaliyomo ni kwamba, polisi wanapaswa kupeleleza kesi kwanza na kukamilisha upelelezi kabla ya kuwakamata watuhumiwa. Hivyo basi, ni vyema jeshi la polisi kuzingatia mapendekezo kama haya ambayo yatasaidia kuepusha usumbufu wa kukamata watu bila upelelezi kukamilika.

 

Imetolewa leo tarehe 5 Machi 2020, na:
Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC)