FCT YABADILISHA UAMUZI WA TCRA DHIDI YA WATETEZI TV: “TCRA HAINA MAMLAKA YA KUTOZA FAINI”

FCT YABADILISHA UAMUZI WA TCRA DHIDI YA WATETEZI TV: “TCRA HAINA MAMLAKA YA KUTOZA FAINI

Dar es Salaam, Tanzania

Leo tarehe 4 Mei 2020, Baraza la Ushindani (FCT) limetoa uamuzi wake kwenye rufaa iliyokatwa na Watetezi TV mnamo Septemba 27, 2019, dhidi ya Kamati ya Maudhui ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

Baraza la Ushindani (FCT) limeamua kuwa Kamati ya Maudhui ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TRCRA) haina mamlaka ya kutoza faini chini ya Kanuni ya 18 ya Kanuni za Mawasiliano ya Kieletroniki na Posta (Maudhui ya Mtandaoni), 2018.

Hapo awali, Kamati ya Maudhui ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) iliwatoza Watetezi TV faini ya Shillingi Millioni Tano za Kitanzania (Tsh 5,000,000/-) kwa kutokuweka Sera au Mwongozo kwa watumiaji wake kwenye mitandao yao ya kijamii kinyume na Kanuni ya 5(1)(c) ya Kanuni za Mawasiliano ya Kieletroniki na Posta (Maudhui ya Mtandaoni), 2018.

Kamati ya Maudhui ya TCRA ilifikia uamuzi huo kulingana na Kanuni ya 18 ya Kanuni za Mawasiliano ya Kieletroniki na Posta (Maudhui ya Mtandaoni), 2018.

Hata hivyo, Watetezi TV haikuridhika na uamuzi huo na hivyo wakakata rufaa mbele ya Baraza la Ushindani kwa sababu tatu;

• Mosi, kwamba kamati ya Maudhui ilikosea kisheria kwa kutumia kifungu kisicho sahihi kufikia uamuzi wake.

• Pili, kwamba Kamati ya Maudhui ilitoa uamuzi huo bila kuwa na mamlaka.

• Tatu, kwamba kamati ilikosea kisheria kwa kushitaki chombo kisichokuwepo.

Dr. Mwenegoha, mwanachama wa Baraza akisoma uamuzi, alikubaliana na sababu ya kwanza ya rufaa kwamba kamati ya Maudhui ilikosea kisheria kwa kutumia kifungu kisicho sahihi kufikia uamuzi wake. Kwani Kanuni ya 18 haitoi mamlaka kwa mamlaka kama Kamati ya maudhui kutoza faini. Hivyo, ilikuwa kosa kwa Kamati hiyo kuwatoza faini kulingana na Kanuni ya 18 kwasababu Kanuni hiyo inatumika pale ambapo mtoa maudhui hukutwa na hatia. Mamlaka ya kumtia mtu hatiani ni ya Mahakama pekee yake. Hivyo kamati ya Maudhui ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) haina mamlaka ya kumtia mtu hatiani.

Hata hivyo, Dr. Mwenegoha alisema kuwa Watetezi TV kwa wakati huo, ilikuwa imekiuka Kanuni ya 5(1)(c) ya Kanuni za Mawasiliano ya Kieletroniki na Posta (Maudhui ya Mtandaoni), 2018 kwa kushindwa kuchapisha Sera au Mwongozo kwa watumiaji wake.

Hivyo, Baraza limefikia uamuzi wa kuweka kando uamuzi uliotolewa na Kamati ya Maudhui ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na kubadilisha adhabu kuwa kulipa faini ya Shilingi Millioni Tatu (3,000,000/-) chini ya kifungu cha 44(2)(b) cha Sheria ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

Sababu nyingine mbili za rufaa zilikubaliwa kwa sehemu na kukataliwa kwa sehemu.

Mnamo, September 25, 2019 Watetezi TV iliitwa na kamati ya Maudhui ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kujibu juu ya shitaka la kutokuweka sera au mwongozo wa watumiaji wa mitandaoni kwenye mitandao yao ya kijamii kinyume na Kanuni ya 5(1)(c) ya Kanuni za Mawasiliano ya Kieletroniki na Posta (Maudhui ya Mtandaoni), 2018.

Kanuni ya 5(1)(c) inasema kuwa “Mtoa Maudhui ya mtandaoni atakuwa na jukumu la kutengeneza sera au mwongozo wa mtandaoni na kuufanya upatikane kwa watumiaji.”

Uamuzi uliotolewa na Baraza siku ya leo umeangaza kuwa Kamati ya Maudhui ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania imeitoza Watetezi TV faini kubwa kinyume na sheria.

Baraza limeeleza pia kuwa, kifungu sahihi cha Sheria kilichopaswa kutumika ni kifungu cha 44(2)(b) cha Sheria ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania. Hata hivyo kifungu cha 44 pia kinakosa viungo muhimu vya kuzingatiwa kabla ya kutoza faini.

Uamuzi uliotolewa na Baraza la Ushindani leo katika rufaa ya Watetezi TV utawasaidia waendeshaji wa vyombo vya Habari vya Mtandaoni kuwa makini katika kutetea haki zao. Pia umamuzi huo umeujulisha Umma kuwa Kamati ya Maudhui ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) haina mamlaka ya kutoza faini kulingana na Kanuni ya 18.

Hivyo, faini yoyote iliyowahi kutozwa na Kamati ya Maudhui ya Mamlaka ya Mawasilano Tanzania (TCRA) haikuwa sahihi kulingana na Kanuni ya 18 na hivyo inapaswa kupingwa mbele ya mamlaka husika kama Baraza la Ushindani.

Zaidi ya hayo, uamuzi wa Baraza la Ushindani umeamsha watunga sheria kufanya mabadiliko husika kwenye Kanuni za Mawasiliano ya Kieletroniki na Posta(Maudhui ya Mtandaoni), 2018.

Kufuatia uamuzi huu wa Baraza la Ushindani dhidi ya Watetezi TV, Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) utapitia uamuzi uliotolewa ili kujiandaa na kuona kama utapeleka rufaa kwenye Mahakama ya Rufaa au la.

Mawakili waliosimama badala ya Watetezi TV kwenye rufaa hii mbele ya Baraza la Ushindani ni; Benedict Ishabakaki, Bertha Nanyaro na Rayson Elijah Luka kutoka Kampuni la Mwakili la Victory Attorneys& Consultants .

Imetolewa na:
Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC),
Tarehe 4 Mei 2020