DPP AJITOA KWENYE KESI YA KUPINGA WATUHUMIWA KUSHTAKIWA KWENYE MAHAKAMA ZISIZOKUWA NA MAMLAKA (COMMITAL PROCEEDINGS)

DPP AJITOA KWENYE KESI YA KUPINGA WATUHUMIWA KUSHTAKIWA KWENYE MAHAKAMA ZISIZOKUWA NA MAMLAKA (COMMITAL PROCEEDINGS)

Dar es Salaam, Tanzania

Kesi ya mwanaharakati anayepinga watuhumiwa kukamatwa na kushtakiwa kwenye mahakama zisizokuwa na mamlaka ya kusikiliza kesi hizo imetajwa leo Juni 03, 2020 mbele ya Jopo la majaji wawili; Jaji Mlyambina na Jaji Magoiga.

Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP) aliwasilisha maombi ya kuunganishwa kwenye kesi hiyo upande wa serikali lakini aliandika barua tena kuomba maombi yake yaondolewe kwenye kesi hiyo kabla hata ya kusikilizwa.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Juni 16, 2020 sa 07:30 mchana kwasababu leo akidi/koramu ya majaji watatu haikutimia.

Mwanaharakati huyo ambaye pia ni Mratibu wa Kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Bw. Onesmo Olengurumwa alifungua kesi namba 36 ya mwaka 2019 (mnamo Desemba 16, 2019) dhidi ya Mwanasheria mkuu wa serikali katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Masijala ya Dar es Salaam akipinga watuhumiwa wa mbalimbali nchini kushtakiwa kwenye mahakama zisizokuwa na mamlaka ya kusikiliza kesi hizo (committal proceedings).

Katika kesi hiyo, Bw. Onesmo anapinga watuhumiwa wa makosa mbalimbali kukamatwa bila upelelezi kukamilika na kushtakiwa kwenye mahakama zisizokuwa na mamlaka ya kusikiliza na kutoa uamuzi kuhusu kesi hizo.

Kesi hiyo ilipangwa kutajwa leo na kupangiwa jaji mmoja wa kusikiliza pingamizi moja la serikali dhidi ya Bw. Onesmo Olengurumwa. Pingamizi hilo liliwasilishwa kipindi kesi hiyo ilipotajwa kwa mara ya pili Februari 25, 2020 ambapo Mwanasheria mkuu wa serikali aliwasilisha pingamizi moja la awali kuwa “kesi ya Bw. Olengurumwa inafanana na kesi nyingine ambayo ilishawahi kutolewa uamuzi na mahakama”.

Lengo la Bw. Olengurumwa kufungua kesi hiyo ni kuiomba Mahakama Kuu ya Tanzania kutoa tamko la kufuta kifungu namba 178, 243, 244, 245, 246, 247, 248, 249, 250, 256, 257, 258 na 259 vya Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai Sura ya 20 (Toleo la mwaka 2002) kuwa ni kinyume na Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania ya mwaka 1977 sababu vinakiuka haki na uhuru wa watuhumiwa, kuminya utawala wa sheria, na kufifisha mchakato mzima wa uendeshaji wa kesi kwa usawa, pia vinahamasisha matumizi mabaya ya mamlaka ikiwemo kufanya upelelezi.

Baadhi ya hoja za Bw. Olengurumwa ni kwamba, mtuhumiwa anapofunguliwa mashtaka kwenye mahakama ambayo haina mamlaka ya kuisikiliza kesi yake, mtuhumiwa huwa haruhusiwi kusema chochote, hivyo humfanya akose haki yake ya msingi ya kusikilizwa kwa wakati.

Pia, Sheria bado haijaweka utaratibu wa namna ya kuhakikisha upelelezi unafanyika haraka na kwa wakati ili kuhakikisha kwamba mtuhumiwa anafikishwa mbele ya mahakama yenye mamlaka ya kusikiliza kesi yake.

Kwa mfano, kifungu namba 178 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai Sura ya 20 (Toleo la mwaka 2002), kinasema kuwa, “pale ambapo kesi itafunguliwa kwenye mahakama ambayo haina mamlaka ya kuisikiliza, baada ya upelelezi kukamilika, mahakama hiyo inapaswa kutoa amri ya kesi hiyo kwenda kusikilizwa kwenye mahakama kuu.

Hivyo, kwakuwa upelelezi umekuwa ukichukua muda mrefu kwenye kesi nyingi ama pengine kutokamilika, kifungu hicho namba 178 kimekuwa hakina uhalisia, hivyo kinastahili kufutwa kabisa.

Ibara ya 64 (5) ya Katiba ya Tanzania ya Mwaka 1977 inaweka bayana kuwa, Bunge linawajibu wa kutunga sheria ambazo hazikinzani na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 na endapo sheria hizo zikikinzana, katiba kwa vile ni sheria mama ndio hutumika.

Imetolewa na:
Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC)
03/06/2020