SALAMU ZA POLE KUFUATIA KIFO CHA MTETEZI WA HAKI WA MUDA MREFU NA MWANA-AZAKi WAKILI EVOD MMANDA – MKUU WA WILAYA YA MTWARA

Wapendwa Wanachama, Familia ya marehemu, Wana-AZAKi na umma wa watanzania kwa ujumla,
Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) umepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha Mtetezi wa Haki za Binadamu wa muda mrefu na mwana-AZAKi Mhe. Wakili Evod Mmanda ambaye pia alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Mtwara. Marehemu alifariki usiku wa kuamkia leo tarehe 27 Aprili 2020 katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Mtwara.
Kwa namna ya kipekee THRDC inatanguliza salamu za rambirambi kwa familia, ndugu, jamaa, marafiki wa marehemu Wakili Evod Mmanda pamoja na watetezi wote wa haki za binadamu nchini waliofikwa na msiba huu.
Historia ya kazi za Utetezi za marehemu Wakili Evod Mmanda
Marehemu Wakili Evod Mmanda ni mmoja wa watetezi wakongwe wa haki za wanawake, haki za umiliki wa ardhi, haki za wafugaji na haki za binadamu kwa ujumla hapa nchini.
Mnamo mwaka 1991, marehemu Wakili Evod Mmanda alianza kazi za utetezi kwa kujitolea kutoa huduma za msaada wa kisheria (Paralegal) katika taasisi changa ya Shirika la Uchumi la Wanawake (SUWATA) lililoanzishwa mwaka 1989. Marehemu alifanya kazi SUWATA katika mradi wao wa Utoaji wa Msaada wa Kisheria kwa wanawake (SUWATA – Legal Aid Scheme for Women) na wakati huo alikuwa mmoja wa watumishi wanne tu waliokuwa wakifanya kazi kwa kujitolea.
Baadaye, mnamo mwaka 1994, marehemu Wakili Evod Mmanda alikuwa mmoja wa waanzilishi wa Kituo cha Msaada wa Sheria kwa Wanawake na Watoto nchini (Women’s Legal Aid Centre – WLAC) kwa kushirikiana na Bi. Hellen Kijo-Bisimba, Mama Nikazaeli Tenga na wengine, ambao walibadilisha SUWATA kuwa WLAC na kufanya kazi pamoja.
Mnamo mwaka 1995, mwaka ambao Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kilianzishwa, LHRC ilimuomba marehemu Wakili Mmanda kuwa Afisa Programu wa LHRC na mkufunzi wa elimu ya haki za binadamu kwa umma kwa muda mfupi na hatimaye kuwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC kwanzia mwezi Septemba 1995 hadi Juni 1996.
Mnamo mwezi Juni mwaka 1996, Bi. Hellen Kijo-Bisimba aliteuliwa rasmi kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, huku marehemu Wakili Evod Mmanda akiendelea kuwa Afisa Programu na mkufunzi wa elimu ya haki za binadamu kwa umma; nafasi yake ya awali.
Marehemu aliendelea kufanya kazi katika Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) hadi mwaka 1999 alipoondoka LHRC na kuwa wakili wa kujitegemea mnamo mwaka 2000. Hata baada ya kuondoka LHRC, marehemu Wakili Evod Mmanda aliendelea kuwa mwanachama hai wa LHRC hadi hapo jana umauti ulipomfika.
Pia kati ya mwaka 2007 hadi 2015, marehemu Wakili Evod Mmanda alikuwa mjumbe wa bodi ya Tanzania Association of NGOs (TANGO) na baadaye kuteuliwa na wajumbe wenzake wa bodi kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya TANGO. Mwaka 2014 pia alikuwa mmoja wa wajumbe wa Bunge la Katiba kupitia shirika la TANGO.
Itakumbukwa pia kuwa katika kipindi hicho, marehemu Wakili Evod Mmanda aliongoza vipindi vya IJUE SHERIA vinavyorushwa hewani na kituo cha runinga cha ITV.
Marehemu Mtetezi Evod Mmanda kama mlezi na mkufunzi wa Haki za Binadamu
Marehemu Mtetezi na Wakili Evod Mmanda atakumbukwa na wengi kama mtetezi wa haki za wanawake na wafugaji. Ila zaidi atakumbukwa kama mwalimu na mlezi (Mentor) wa wanaharakati mashuhuri nchini kama Mama Jane Magigita – Mkurugenzi wa Equality for Growth, ambapo kati ya miaka ya 1997 hadi 1998 walifanya kazi pamoja katika Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kwenye mradi wa kutoa mafunzo ya haki za umiliki wa ardhi kwenye jamii za wafugaji za kimaasai Wilaya za Hanang, Simanjiro, Milerani na kwingineko nchini.
Uteuzi wa Marehemu kwenye Ulingo wa Siasa
Baada ya kumaliza muda wake kama Mwenyekiti wa bodi ya TANGO mwaka 2015, baadaye marehemu Evod Mmanda alijikita na siasa na kuwa mwanachama wa NCCR-Mageuzi na baadaye kuhamia Chama Cha Mapinduzi (CCM). Hatimaye mnamo mwaka 2016, Marehemu Wakili Evod Mmanda aliteuliwa na Rais John Pombe Magufuli kuwa Mkuu wa Wilaya ya Mtwara hadi hapo jana umauti ulipomfika.
Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu Wakili Evod Mmanda, mtetezi nguli wa haki za wanawake na wafugaji. Tutakumbuka daima mchango wako kwenye Sekta ya Asasi za Kiraia nchini.
Pumzika kwa Amani! Bwana ametoa, Bwana ametwaa, jina lake lihimidiwe. Amina!
Imetolewa na: Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) 
Leo tarehe 27 Aprili 2020