TANZIA!!!
THRDC YAMPOTEZA MTETEZI BI. DEBORAH DAFFA, MWANZILISHI WA TANGA PARALEGAL CENTRE
Wapendwa wanachama,
Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) pia umepokea kwa huzuni kubwa taarifa ya kifo cha mwanachama wake Mkurugenzi wa Shirika la Tanga Paralegal Bi. Debora Dafa kilichotokea juzi jioni tarehe 16/4/2020, katika Hospitali ya Magunga Wilayani Korogwe alipokuwa akipatiwa matibabu baada ya kuugua ghafla.
Msiba upo nyumbani kwa marehemu mtaa wa Sahare mkoani Tanga.
HISTORIA YA HARAKATI ZA MTETEZI MWENZETU MAREHEMU BI. DEBORAH DAFFA
Bi. Deborah Daffa, alizaliwa mnamo tarehe 14/02/1942 huko kijijini kwao Ambangulu Wilaya ya Korogwe Mkoani Tanga. Bi. Debora Daffa aliwahi kuwa Mwalimu wa Shule za Msingi mbalimbali Mkoani Tanga na kushika nyadhifa mbalimbali kwenye sekta ya Elimu nchini. Marehemu aliwahi kuwa Mratibu wa Elimu Mkoani Tanga.
Marehemu Bi. Debora Daffa alianza harakati za utetezi wa haki za binadamu hasa kutetea haki za Wanawake na Watoto tangu alipokuwa Mwalimu. Alitumia muda wake mwingi kuwapa elimu watoto juu ya haki zao za msingi na jinsi ya kukabiliana na vitendo vya ukatili. Pia katika harakati zake, alikuwa bega kwa bega na wanawake wanaopitia changamoto za ukatili majumbani pamoja na kuwapa msaada wa kisheria bure na hata kuwapeleka kwenye vituo vya msaada wa kisheria. Marehemu Bi. Debora Daffa alijizolea umaarufu mkubwa Mkoani Tanga kwa utoaji wa msaada wa kisheria.
Mnamo nwaka 1992, Bi. Debora Daffa alipata fursa ya kupata mafunzo kutoka shirika la WLAC. Mafunzo hayo yalimjenga katika harakati za kutetea haki za binadamu na unyanyasaji wa kijinsia pamoja na kupinga ukiukwaji wa sheria kwa wanawake na watoto.
Hii ilimpelekea yeye na wenzake waliopata mafunzo hayo kuanzisha kwa pamoja KITENGO CHA KUTOA MSAADA WA SHERIA KWA AKINA MAMA NA WATOTO, mnamo mwaka 2003 chini ya Sheria ya Registration Incorporation Trustees Act (RITA). Baadae kitengo hiki kilisajiliwa upya mnamo tarehe 15/07/2011 kama Tanga Paralegal for Women and Children mkoani Tanga.
Ikumbukwe kuwa, Bi. Debora Daffa ni mmoja wa wanawake waanzilishi wa TANGA PARALEGAL ikiwa ni kituo cha kwanza cha msaada wa kisheria kuanzishwa nchini Tanzania. Tanga Paralegal ni maarufu kwa kutoa msaada wa kisheria bure kwa wanawake na watoto mkoani Tanga.
Bi. Debora Daffa katika harakati zake za utetezi wa haki za wanawake na watoto aliamini kuwa mwanamke ni kiungo muhimu katika nyanja zote za maendeleo katika jamii na taifa kwa ujumla. Na pia alipambania kutoa elimu kwa jamii kuhusu kulinda na kuheshimu haki za binadamu hasa wanawake na watoto. Bi. Debora Daffa pia alipambania haki za mirathi za wajane wenzake waliodhurumiwa mali zao baada ya waume zao kufariki. Kupitia shirika la Tanga Paralegal alilokuwa akiliongoza kama mmoja ya waanzilishi na Mkurugenzi, lilipata umaarufu.
Pia mnamo mwaka 2016, marehemu Bi. Debora Daffa, kupitia shirika la Tanga Paralegal alijiunga kuwa mwanachama wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC). Kupitia THRDC, Bi. Debora Daffa alihudhuria mafunzo mbalimbali ya kisheria na mafunzo mengine ya Usalama kwa watetezi tuliyokuwa tukiyatoa na kutunukiwa vyeti mbalimbali vya kufuzu mafunzo hayo. Mafunzo hayo yalimfanya akomae na kupambana kiustadi katika kutetea haki za binadamu kwa ujumla.
Marehemu Bi. Debora Daffa almaarufu kama IRON LADY enzi za uhai wake, alikuwa mtetezi na mpambanaji katika kukataa kunyanyaswa, kunyimwa haki na kudhulumiwa haki. Alisimamia HAKI, USAWA WA KIJINSIA, na pia ALIKUWA MAMA IMARA.
Pumzika kwa Amani Bi. Debora Daffa, Mtetezi mwenzetu na Mkurugenzi wa Tanga Paralegal na mwanachama wa Mtandao wa watetezi wa haki za Binadamu Tanzania (THRDC).
Bwana ametoa na Bwana ametwaa jina lake lihimidiwe. Amina!
N.B: Wapendwa wanachama tanaomba tuungane pamoja kuiombea faraja familia ya marehemu pamoja na watetezi wengine waliofiwa katika kipindi hiki.
Imetolewa na;
Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC)